Watu wawili wanaosadikiwa kuwa ni miongoni mwa wahalifu wanaoendesha mauaji katika Kanda Maalumu ya Kipolisi Rufiji wameuwa na Jeshi la Polisi.
Mmoja wa watu hao ametambulika kwa jina la Abdallah Ally Ngande Makeo ambaye alikuwa anatafutwa na Jeshi la Polisi kwa muda mrefu kutokana na kushiriki kwake katika matukio ya mauaji maeneo ya Ikwiriri, Kibiti pamoja na uvamizi wa kituo cha Polisi Ikwiriri.
Mkuu wa Operesheni Maalum za Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi, Liberatus Sabas amesema kuwa tukio hilo lilitokea mnamo tarehe 19, julai, 2017 saa mbili usiku katika eneo la Utende kata ya Ikwiriri, wilaya Rufiji Kanda Maalum ya Polisi Rufiji.
Aliongeza kuwa katika eneo hilo la tukio ilipatikana silaha moja aina ya rifle 375 ambayo ilikutwa imekatwa kitako na mtutu ikiwa na risasi mbili (2).
Miili ya marehemu wote wamehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Kamanda sabas ameendelea kutoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kutoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa wahalifu wengine waliosalia na kwamba opereheni hiyo ya kuwasaka wahalifu katika Kanda hiyo ya kipolisi Rufiji ni endelevu na hakuna atakaye baki.