Maelfu ya watu wamejitokeza katika barabara za kuelekea nyumbani kwa Bradley Lowery, shabiki wa klabu ya Sunderland FC ya Uingereza, kutoa heshima zao za mwisho.
Lowery, mwenye umri wa miaka sita, alitoka Blackhall Colliery, County Durham ambapo alifariki Ijumaa wiki iliyopita baada ya kuugua saratani kwa muda mrefu.
Mchezaji Jermain Defoe, ambaye aliunda urafiki wa karibu sana na Bradley, aliungana na familia ya mvulana huyo kumuaga kwa mara ya mwisho.
Ibada ya wafu ilifanyika katika kanisa la Mtakatifu Yusufu kijijini mwao, wengi wakimsifu sana mvulana huyo kwa ukakamavu wake na sifa alizojilimbikizia.
Barabara za kuelekea kanisa la Mtakatifu Yusufu zilipambwa kwa puto na mabango yenye ujumbe wa kutoa heshima kwa Lowery.
Wengine waliacha ujumbe nje ya uwanja wa Sunderland wa Stadium of Light na waombolezaji walifika kwa wingi kanisani, hivi kwamba wengine walikaa nje.
Mamake Gemma aliambia waliohudhuria mazishi hayo: “Alikuwa na tabasamu kubwa na la kupendeza hivi kwamba lilikuwa lingeangaza chumba chochote kile. Ni shujaa mwenye ujasiri, ametuacha.
Bradley alikuwa anaugua ugonjwa ambao kwa Kiingereza hufahamika kama neuroblastoma – aina nadra ya saratani tangu alipokuwa na umri wa miezi 18.
Bradley alifanywa kuwa kibonzo-nembo wa klabu hiyo na akaunda urafiki wa karibu na mshambuliaji wa klabu hiyo Jermain Defoe.
Aidha, aliongoza wachezaji wa England kuingia uwanjani Wembley wakati wa mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia dhidi ya Lithuania.
Bradley alipewa matibabu lakini saratani yake ikaibuka tena mwaka jana.
Wahisani walichangisha zaidi ya £700,000 kulipia matibabu yake New York mwaka 2016, lakini madaktari waligundua kwamba saratani yake ilikuwa imeenea sana na hangeweza kutibiwa.