Diwani wa kata ya Ngabobo (Chadema), Solomon Laizer amejiuzulu udiwani na kujiunga na CCM kwa maelezo kwa ajili ya kumuunga mkono Rais John Magufuli.
Laizer ni diwani wa tano katika Halmashauri ya Meru kujiuzulu kwa kutoa sababu kuwa anamuunga mkono Rais Magufuli.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Christopher Kazeri amethibitisha leo kupata taarifa za kujiuzulu kwa Ngabobo.
Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari amesema kujiuzulu kwa diwani huyo ni mchezo mchafu akidai amenunuliwa.
Amesema tayari walipata taarifa za diwani huyo kushawishiwa kujiuzulu na kwamba, alifuatwa na viongozi wa wilaya na kanda wa chama hicho aliowaeleza kuwa ameshawishiwa.
Hadi sasa madiwani watano wa Chadema waliojiuzulu ni Credo Kifukwe wa Kata ya Murieti jijini Arusha.
Wengine waliojiuzulu katika Jimbo la Arumeru Mashariki na kata zao kwenye mabano ni Anderson Sikawa (Leguruki), Emmanuel Mollel (Makiba), Greyson Isangya (Maroroni) na Josephine Mshiu (Viti Maalumu).