Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesema kuwa Halima Mdee alielezea hisia zake kama mwenyekiti wa Baraza la wanawake la Chadema Taifa.
Mbowe amesema hayo katika viwanja vya mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya mbunge wa Kawe, Halima Mdee kuachiwa kwa dhamana.
Mwenyekiti huyo ambaye ni mbune wa Hai amesema kuwa Mdee alieleza kuhusu hisia zake na sio vinginevyo kuhusu agizo la Rais Magufuli kuwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari watakaopata ujauzito hawataruhusiwa kuendelea na masomo.
Mdee alishikiliwa na jeshi la polisi kwa siku tano kufuatia amri ya kukamatwa iliyotolewa na mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi baada ya kudaiwa kutoa maneno ya kashfa dhidi ya Rais John Magufuli. Mdee alifikishwa mahakamani akikabiliwa na shtaka la kumkashfu Rais.
“Sisi kama chama na kama viongozi, tunaamini kila Mtanzania awe kiongozi asiwe kiongozi, wa chama chochote na wa dini yoyote ana haki ya kueleza hisia zake.
Mwenyekiti huyo wa Chadema aliongeza kuwa chama chake kitaendelea na mjadala huo bila kujali hatua za kisheria zitakazochukuliwa dhidi yao.