Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-Un amemkejeli Rais wa Marekani, Donald Trump saa chache baada ya kufyatua kombora zito ambalo linadaiwa kuwa na uwezo wa kufika nchini Marekani.
Timu ya ujasusi ya Marekani ilieleza kuwa kombora hilo la Korea Kaskazini lililofyatuliwa wiki hii limeonesha kufanikiwa kwa kiasi kikubwa na kwamba lilienda umbali wa zaidi ya Kilometa 900 kabla halijatua baharini kwenye eneo muhimu la kiuchumi nchini Japan.
Kim Jong-Un ameeleza kuwa kombora hilo lililofyatuliwa Julai 4, siku ya kuadhimisha uhuru wa Marekani, lilikuwa zawadi yake kwa Marekani na kiongozi wake.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Marekani imeeleza kuwa Rais Trump na timu ya wana usalama inaendelea kuvifanyia usaili wa karibu vitendo vya Korea Kaskazini na kwamba nchi hiyo imefikia ukomo wa uvumilivu wake.
Imeeleza kuwa Marekani itaongeza vikwazo zaidi dhidi ya nchi hiyo wakati ambapo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likitarajiwa kujadili hatua dhidi ya Korea Kaskazini.
Urusi na China, jana zilitoa tamko la kulaani majaribio ya makombora yanayofanywa na Korea Kaskazini, ambayo ni tishio kwa dunia nzima.
Kombora hilo aina ya Hwasong -14 liliruka umbali wa kilomita 2,802 na kusafiri kwa umbali wa kilomita 933 kwa dakika 39 kabla ya kuanguka baharini.
Korea Kaskazini imesema kuwa ni taifa lililojihami kinyuklia ambalo linamiliki kombora la masafa marefu linaloweza kushambulia eneno lolote duniani.