Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la soka imetangaza kuwa mchakato wa uchaguzi mkuu wa shirikisho hilo umesimamishwa hadi Kamati ya Utendaji itakapokutana Julai 4, mwaka huu.
Tamko hilo limetolewa katika mkutano na waandishi wa habari leo Jumapili mchana kwenye Ofisi za TFF zilizopo Karume jijini Dar es Salaam.
Imeelezwa uamuzi huo umechukuliwa baada ya wajumbe wa kamati ya uchaguzi kukiuka taratibu.
Tayari zoezi la usaili wa wagombea wa nafasi mbalimbali ikiwemo urais lilikamilika jana Jumamosi tangu lilipoanza Alhamisi iliyopita huku wagombea wawili wakikosekana akiwemoRais wa TFF, Jamal Malinzi ambaye anatetea nafasi yake ya urais na Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ anayewania nafasi ya Makamu Rais wa TFF kutokana na wahusika hao kuwa rumande.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku moja baada ya wajumbe wa Kamati hiyo kudaiwa kufanya juhudi ili Malinzi afanyiwe usaili licha ya kuwa mahabusu wakati ambapo inaelezwa Kaburu aliandika barua ya kujiondoa kwenye mchakato wa uchaguzi.