Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amekubali ameachia ngazi katika nafasi ya kiti hicho.
Hatua hiyo imekuja mara baada ya kiongozi huyo kuwekwa rumande hadi Julai 3, mwaka huu baada ya kusomewa mashtaka yake mahakamani hapo jana, jambo ambalo litamfanya akose nafasi ya kuhudhuria katika zoezi la usaili wa wagombea ambalo litafungwa kesho Julai Mosi.
Malinzi amezungumza kupitia wakili wake, Aloyce Komba kwamba anawashukuru watanzania kwa ushirikiano waliompa katika kipindi chote akiwa Rais, na kuwataka waelewe kuwa Soka la Tanzania bila Malinzi linawezakana.
Rais huyo anayekabiliwa na mashtaka takriban 28 yakiwemo ya utakatishaji wa fedha na kughushi nyaraka, amewataka wajumbe kuchagua mtu mwingine kwani anaamini kuwa kuna watanzania wengi wenye uwezo wa kuliongoza soka la Tanzania.
Hata ivyo Kauli hiyo inaashiria kukubali kuachia nafasi hiyo ya urais, ikizingatiwa pia mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Revocatus Kuuli alikwishaweka msimamo kuwa mchakato wa uchaguzi hautasimama, na kwamba yeyote ambaye hatatokea kwenye usaili atakuwa amejiengua mwenyewe.