Mwanamuziki mkongwe nchini Uganda, Robert Kyagulanyi Ssentamu, maarufu kama Bobi Wine ameshinda ubunge katika uchaguzi mdogo nchini humo.
Bobi Wine ambaye aliwania kama mgombea huru aliwashinda wagombea wengine wanne katika eneo bunge la Kyadondo Mashariki katikati mwa Uganda.
Alipata kura 25,659 kutoka kwa kura 33,310 zilizopigwa dhidi ya wapinzani wake katika jimbo hilo nchini Uganda.
Baada ya kutangazwa ushindi Bobi Wine amesema kuwa “Jambo langu la kwanza ninalotaka kufanya ni kufanikisha maridhiano kati ya viongozi wa Kyadondo Mashariki…Ninataka siasa zitulete pamoja… jinsi muziki ufanyavyo.”
Mwanamuziki huyo alikuwa amekamatwa na polisi na kuhojiwa kwa muda kabla ya kuachiliwa siku chache zilizopita.
Kiti hicho cha ubunge kiliachwa wazi baada ya mahakama kuamua kuwa uchaguzi uliofanyika mapema mwaka jana haukufuata kanuni na sheria za uchaguzi.
Kiongozi wa chama cha upinzani cha FDC Kizza Besigye amempongeza mwanamuziki huyo kwenye Twitter.
Ameandika: „Ushindi mkubwa kwa Mheshimiwa Bobi Wine. Hongera – Nguvu za Raia!! Ndio maana watu wa Wakiso hawakuruhusiwa kupiga kura mwaka 2016.”