Wakala wa barabara Tanzania (Tanroads), umesema muda wowote kuanzia wiki ijayo wanatarajia kuanza utekelezaji wa kubomoa nyumba zilizowekewa alama ya X katika barabara ya Morogoro kuanzia Kimara, jijini Dar es Salaam.
Meneja wa wakala huo Mkoa wa Dar es Salaam, Julius Ndyamukama alisema hayo jana wakati akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu na kuongeza kuwa wanakamilisha taratibu za mwisho ili kuanza utekelezaji wa ubomoaji wa nyumba hizo.
Kuhusu fidia alisema hakuna atakayepewa fidia na taarifa za kutosha kuhusu bomoabomoa hiyo wanayo wakazi wa eneo hilo, tatizo ni kwa wale ambao huwa hawaamini hadi hapo wanapokuwa wameona polisi na vijiko vikibomoa.
Alisema bomoa hiyo inatekelezwa katika mita 121 kutoka katikati ya barabara kwa kila upande wa barabara na itaanza kubomolewa kuanzia Kimara Stopover mpaka Kiluvya kwa lengo la kupisha mradi wa ujenzi wa upanuzi wa barabara ya Morogoro.
Amesema hifadhi ya barabara ya Morogoro ina upana wa mita 121.5 kutoka katikati mwa barabara kila upande. Alisema wakazi hao wanatakiwa kubomoa nyumba hizo ndani ya siku 30 kuanzia siku walipopewa notisi na kwamba watakaokaidi nyumba zao zitabomolewa na watalazimika kulipa gharama zote zitakazojitokeza katika utekelezaji wa hatua hiyo.
Katika uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini baadhi ya wakazi wanaotakiwa kubomoa nyumba zao kuanzia eneo la Kimara Stopover wameanza kutekeleza agizo hilo wenyewe na maeneo mengine kukiwa kumebakia mapagala.
Amesema baadhi ya waliowekewa alama wameshaondoka, lakini pia hata wenye maduka wamekuwa waoga kufungua na wengine tayari wameondoka na kuhamishia biashara zao maeneo mengine.