Mjumbe wa kamati ya Chadema, Edward Lowassa amemtaka Rais Magufuli kutafakari hatima ya masheikh wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumuki) maarufu ‘Uamsho’ wanaosota gerezani kwa miaka minne sasa bila kesi yao kuamuliwa.
Masheikh hao ambao wamefunguliwa kesi ya ugaidi, awali kesi yao ilikuwa ikiendeshwa katika Mahakama Kuu ya Zanzibar na baadaye kuhamishiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam inakoendelea hadi sasa.
Lowassa amesema ni jambo la fedheha kwa nchi iliyopata uhuru zaidi ya miaka 50 kuwaweka mahabusu viongozi wa dini muda mrefu kiasi hicho bila kesi kusikilizwa mahakamani.
Amesema kama masheikh hao wamefanya makosa wapelekwe mahakamani ili haki itendeke lakini kuendelea kuwashikilia ni fedheha kubwa kwa Taifa.
Waziri Mkuu huyo wa zamani alisema kama ambavyo Rais Dk. John Magufuli, ametekeleza ahadi ya vyama Vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa kuunda Tume mbili za kushughulikia madini ya dhahabu, hana budi kutekeleza na ahadi yake (Lowassa) kuwatoa kizuizini masheikh hao wa Uamsho.
Akizungumzia suala la kuenzi amani ya nchi aliwataka waumini wa dini ya Kiislamu wanapotafakari mambo mbalimbali kupitia mwezi Mtukufu wa Ramadhan wakemee jambo hilo ambalo alisema linavurugwa na chuki zikiwamo za kisiasa.