Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Simon Sirro amesema mauaji ya polisi, viongozi na raia katika maeneo ya Kibiti, Rufiji na Ikwiriri ni ya muda na kusisitiza majibu yake yako mbioni kupatikana.

Sirro ametoa kauli hiyo jana katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Moshi (MPA), wakati wa kufunga mafunzo ya upandishaji vyeo kwa maofisa na askari 222 wa Jeshi la Uhamiaji nchini.

Kauli ya Sirro imekuja huku kukiwa na mfululizo wa mauaji ya polisi na raia katika maeneo hayo ambapo zaidi ya watu 35 wameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana wakiwamo polisi 13.

Hadi sasa, licha ya polisi kufanya operesheni kubwa katika maeneo hayo, bado halijaweza kubaini chanzo cha mauaji hayo na kwa nini wanawalenga polisi na baadhi ya watu na nani wanayatekeleza.

Tukio la hivi karibuni kabisa lililotokea Jumatano iliyopita, ambapo watu wasiojulikana waliwashambulia kwa risasi na kuwaua polisi wawili wa kikosi cha usalama barabarani huko Kibiti.

Akizungumza katika sherehe za kuhitimu mafunzo kwa maofisa na askari hao 222 wa Jeshi la Uhamiaji, Sirro amesema japokuwa nchi ni salama, lakini inakabiliwa na kitisho cha usalama eneo hilo.

Akizungumzia changamoto zinazolikabili Jeshi la Uhamiaji, Sirro aliyekuwa mgeni rasmi amesema moja ya changamoto kubwa ni uingiaji wa wahamiaji haramu wanaopitia njia zisizo rasmi kuingia nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *