Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba amewaagiza wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi kuwadhibiti maofisa watendaji wa vijijiji na kata ambao wamekuwa wakitafsiri tofauti maagizo ya viongozi na kufanya maamuzi yanayowaumiza wananchi.
Akizungumza kwenye kikao cha siku moja kilichowakutanisha wabunge wa mkoa wa Iringa, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Iringa na wilaya zote pamoja na viongozi wa Serikali za Mitaa na madiwani, alisema maamuzi yao yamekuwa yakiwalazimu wananchi kuichukia Serikali na CCM.
Kikao hicho kilikuwa maalumu kwa ajili ya kutoa msimamo na mapendekezo ya Serikali kuhusu kilimo cha umwagiliaji kinachofanywa kwenye maeneo yaliyokaribu na vyanzo vya maji lengo likiwa kuokoa uharibifu wa vyanzo hivyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masena alisema hakuna mtendaji atakayepona endapo atagundulika kutekeleza shughuli za serikali kinyume na utaratibu.
Akizungumza kwa niaba ya wabunge wenzake Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Venance Mwamoto aliipongeza Serikali kwa uamuzi huo wa kuwataka wale waliokwishalima maeneo yaliyokaribu na vyanzo vya maji kuendelea na shughuli zao hadi hapo Serikali itakapokamilisha mchakato wa kutambua na kubaini maeneo yanayostahili kuachwa.