Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita ameshauri kuanzishwa kwa vilabu vya usalama barabarani mashuleni ili kupunguza ajali na vifo vinavyowapata wanafunzi wanapovuka barabara wakati wa kwenda au kutoka shuleni.
Mwita alitoa kauli hiyo jana wakati akizindua Wiki ya Kimataifa ya Usalama Barabarani kwenye Shule ya Msingi Olympio iliyoandaliwa na Taasisi ya Mashindano ya Magari (AAT) pamoja na Shirikisho la Kimataifa la Mashindano ya Magari (FIA).
Mwita pia alitaka mabasi ya shule yawe yanawachukua na kuwashusha wanafunzi ndani ya kuta za shule badala ya nje kani kufanya hivyo kunawalazimu watoto kuvuka barabara, jambo ambalo linaweza kuleta hatari kwa wanafunzi.
Katika hatua nyingine, Mwita alizishauri AAT na FIA kuendeleza kampeni za kutoa elimu ya usalama barabarani kwa wanafunzi katika shule zote ikiwemo za mikoani. Mwita pia aliwataka walimu pamoja na shule kwa ujumla kutumia kwa umakini vifaa vilivyotolewa katika mitaala yao ya kufundishia masuala ya usalama barabarabani.
Kwa upande wake, Rais wa AAT, Nizar Jinani alishauri barabara zote za jijini Dar es Salaam zilizo karibu na mashule ziwekewe alama za vivuko vya waenda kwa miguu ili kuwepo na sehemu maalumu zitakazotumiwa na wanafunzi kuvuka na hivyo kupunguza ajali. Rais huyo pia aliwataka wanafunzi kuzingatia sheria za usalama barabarani wakati wanapovuka barabara.