Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imeahirisha kesi ya mfanyabiashara maarufu, Shabani Hussein (44) “Ndama mtoto ya Ng’ombe” hadi Julai 20, mwaka huu kwa sababu upelelezi bado haujakamilika.

Shauri hilo lilikuja jana mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Victoria Nongwa, upande wa mashtaka ukisimamiwa na wakili Shedrack Kimaro, wakati wa utetezi ukiongozwa na mawakili wawili Wabaya Kung’e na Nashon Nkungu.

Kwa upande wa utetezi uliwataka Jamhuri kufuatilia upelelezi wa shauri hilo ili kujua kama upelelezi umefikia hatua gani.

Mwanzoni mwa wiki hii Ndama alifanikiwa kutimiza vigezo vya dhamana vilivyomtaka kuwa na wadhamini wawili watakaoweka saini ya maandishi Sh milioni 600 au kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha.

Katika mashtaka hayo, Ndama anadaiwa kuwa kati ya Februari 26 na Machi 2014, Dar es Salaam, akiwa mwenyekiti na mtia saini pekee wa Kampuni ya Muru Platinum Tanzania Investment Limited na akaunti ya benki ya kampuni hiyo iliyoko kwenye Benki ya Stanbic, alijihusisha moja kwa moja kwenye uhamishaji wa dola za Marekani 540,000 na kuzitoa huku akijua fedha hizo ni zao la kosa la uhalifu la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *