Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anatarajia kuwa mgeni rasmi katika mchezo wa kirafiki kati ya Timu ya Everton ya nchini Uingereza na timu ya Gor Mahia ya Kenya.
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amekubali ombi hilo baada ya Kukutana na kufanya mazungumzo na Watendaji wa Kampuni ya SportsPesa Ikulu jijini Dar ess Salaam.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amepongeza mipango na mikakati mizuri ya kampuni hiyo ya kutaka kukuza vipaji vya wanamichezo hasa kwa mpira wa miguu kwa Tanzania Bara na Zanzibar.
Makamu wa Rais pia amewahakikishia watendaji wa kampuni hiyo kuwa milango ya ofisi yake ipo wazi na pindi wakiwama katika jambo lolote wawasiliane na ofisi yake ili tatizo linalowakabili liweze kutafutiwa ufumbuzi ili lisikwamishe shughuli za kampuni hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Utekelezaji wa Kampuni ya Sports Betting nchini Tarimba Abbas amemweleza Makamu wa Rais kuwa kampuni hiyo ina malengo makubwa ya kufanya biashara hapa nchini kwa kuzingatia sheria na kanuni za nchini.
Mkurugenzi huyo Tarimba Abbas amesema katika mipango yao wanataka katika kipindi cha miaka Mitatu ijayo kampuni yao iwe ni moja ya kampuni bora nchini katika ulipaji wa kodi kwa Serikali kama wanavyofanya kwa sasa katika Serikali ya Kenya.
Amesema mipango na mikakati waliyonayo kwa sasa ni kuhakikisha wanainua vipaji vya wanamichezo nchini kwa sababu Tanzania Bara na Zanzibar kuna vipaji vingi vya wachezaji wa mpira wa miguu ambavyo haviendelezwi ipasavyo.