Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe amesema Serikali isipoifutia leseni ya uchimbaji madini Kampuni ya Mwabangu, ataungana na wananchi na kuwaruhusu wang’oe mabati katika Chuo cha Madini wagawane.
Akichangia bajeti kuu ya Serikali ya mwaka 2017/18, Bashe alisema: “Naomba kuwaambia wabunge wenzangu, Watanzania wanapokwenda kuchagua viongozi na wanapokwenda kupiga kura ya kumchagua rais, wanamkabidhi dhamana juu ya uhai wao, usalama wao, anakuwa mlinzi wa rasilimali zao walizopewa na Mungu.
Bashe amesema kuwa “Rais ameunda tume mbili na ametusomea matokeo ya tume, lakini nyuma marais waliotangulia nao waliunda tume mbalimbali, vita ya kupambania rasilimali za nchi hii si ya Rais Magufuli peke yake, ni ya Watanzania wote, hakuna kufanya kosa katika kufanya jambo jema.
Pia amesema kuwa “Bunge limefanya makosa, viongozi wetu wamefanya makosa, leo tumepata mtu wa kupigania rasilimali zetu, tumuunge mkono, akishindwa kutufikisha mwisho tumnyooshee mkono.
Ameongeza kwa kusema kuwa “Resolute wana mgogoro wa kodi na TRA, nataka katika majumuisho mniambie kuhusu Sh bilioni 10 za Nzega tutazipataje.
Mwisho amesema kuwa “Nitamuunga mkono Rais Magufuli katika jitihada zake zote, kile chuo mlichofungua cha madini naenda kuwaambia wananchi wang’oe mabati wagawane.