Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari amemwagia sifa Rais Magufuli kwa hatua anazochukua kuhusu sakata la usafirishaji wa mchanga wa madini (Makinikia).
Kauli hiyo ya Profesa Safari imekuja siku chache baada ya Rais Magufuli kupkea ripoti ya pili kuhusu mchanga wa madini (Makinikia) yaliyopo kwenye makontena hapa nchini.
Profesa Safari amempongeza Rais John Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya kutetea rasilimali za nchi.
Pia amesema kuwa Rais Magufuli anafanya kazi kama walivyokuwa wanafanya baadhi ya viongozi wazalendo barani Afrika ya kupigania haki za wananchi wao kufaidika na rasilimali za nchi.
Profesa Safari aliwaomba Watanzania na wataalamu wa sheria za mikataba, kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais katika kutetea maslahi ya Taifa.
Profesa Safai amemfananisha Rais John Magufuli na Rais wa Kwanza wa Ghana, Kwame Nkrumah na Waziri Mkuu wa Kwanza wa Congo (DRC), Patrice Lumumba kutokana na juhudi binafsi anazofanya kutetea rasilimali za nchi.