Rais wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani, Dkt. John Pombe Magufuli amewaagiza wakuu wote wa mikoa Tanzania Bara kuongeza juhudi za utatuzi wa migogoro ya ardhi.

Rais Magufuli pia amewata wakuu wa mikoa hao kuharakisha mchakato wa kuwanyang’anya hati za umiliki watu wenye mashamba makubwa ambayo hawayaendelezi.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo jana Ikulu Jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Wakuu hao wa mikoa ya Tanzania.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Mcheche Masaju, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi na baadhi ya Mawaziri.

Pia Rais Magufuli amewaagiza Wakuu wa Mikoa wote kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa mpango wa ujenzi wa viwanda katika maeneo yao ili kuwawezesha wananchi kuongeza thamani ya mazao yao na kuzalisha ajira.

 Rais Magufuli amesema kila Mkuu wa Mkoa anapaswa kufanyia kazi fursa za uanzishaji wa viwanda katika eneo lake na kuhakikisha anashawishi wawekezaji kuzitumia fursa hizo.

Rais Magufuli amewataka wakuu wa mikoa hiyo kuiga Mkoa wa Pwani ambako tangu Awamu ya Tano iingie madarakani viwanda vikubwa 83 vimejengwa na vingine kukamilika huku viwanda vidogo zaidi ya 120 pia vikiwa vimejengwa.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *