Matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika jana nchini Uingereza yanaonyesha wazi kuwa hakuna chama kitakachopata ushindi mkubwa wa wabunge wa kukiwezesha kuunda serikali peke yake.
Hili ni pigo kwa Waziri Mkuu, Theresa May aliyeitisha uchaguzi wa mapema akiamini kuwa atapata uungwaji mkono na kuaminiwa, ili aweze kuongoza serikali peke na kuepuka serikali ya muungano.
Hakufanikiwa. May na chama chake cha Conservative anatarajiwa kupata ushindi wa viti 318, huku kile cha Labour kikitarajiwa kupata 262. Hadi asubuhi leo Ijumaa, Conservative ilikuwa na viti 314 na Labour 261 huku Bunge zima likiwa na wabunge 650.
Waziri Mkuu May amesema baada ya matokeo ya mwisho kutangazwa, kutakuwa na muda wa uthabiti huku kiongozi wa Chama cha Labour, Jeremy Corbyn akimtaka May ajiuzulu.
Conservative ilikuwa inahitaji viti 326 ili kuongoza serikali peke yake, lakini kwa namna mambo yalivyo, itabidi kupata uungwaji mkono kutoka chama kingine ili kuunda Serikali.
Haijafahamika iwapo May ataendelea kuongoza chama hicho kutokana na matokeo haya mabaya, kinyume na matarajio yake au atajiuzulu.
Kazi kubwa iliyo mbele ya serikali mpya itakayoundwa ni kuendeleza na kufanikisha mchakato wa kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya.