Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika bejeti yake ya mwaka wa fedha 2017/18 imesema kuwa itawapatia vitambulisho maalumu vya kazi wafanyabiashara wadogo wadogo maarufu kama ‘Machinga’.
Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango wakati akiwasilisha bajeti ya mwaka wa fedha 2017/18 amesema mbali na kupatiwa vitambulisho maalum pia watatengewa maeneo ya kufanya kazi zao.
wafanyabiashara hao watakaopatiwa vitambulisho ni pamoja na mama lishe, wauzaji mitumba wadogo, wauza mazao ya kilimo wadogo kama mboga mboga, ndizi, matunda na kadhalika.
Akizungumzia kuhusu kufungwa kwa biashara, Dk. Mpango alisema jumla ya biashara 7,277 zilifungwa katika mikoa mbalimbali nchini kwa mwaka wa fedha unaomalizika Juni 30.
Alisema suala hilo lilizungumzwa sana na wananchi na wabunge kutokana na kasi ya kufungwa kwa biashara hususan eneo la Kariakoo katika Jiji la Dar es salaam na katika miji mingine.
Amebainisha kuwa mwenendo huo kwa ujumla siyo mzuri kwasababu wananchi wanapoteza ajira na kipato, serikali inakosa mapato ya kodi na uchumi unadorora.
Alisema ni muhimu pale wimbi la kufungwa kwa biashara linapotokea jitihada zifanyike kuelewa aina gani za biashara zinafungwa, kwanini zinafungwa na hatua gani zichukuliwe kudhibiti hali hiyo.