Serikali ya Jamuri ya Muungano wa Tanzania imewasilisha bajeti yake kwa mwaka wa fedha 2017/18, huku ikiwa imetangaza kufuta na kupunguza tozo, ushuru na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye sekta mbalimbali hapa nchini.
Bajeti hiyo imewasilishwa jana na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango ambapo amependekeza kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye bidhaa za mtaji ili kupunguza gharama za mashine na mitambo kwa ajili uanzishwaji wa viwanda vidogo na vya kati, kwenye bidhaa zinazosafirishwa nje ya nchi kuifanya Tanzania iwe njia bora ya kupitisha bidhaa na kuongeza mapato kupitia bandari pamoja na kwenye vyakula vya mifugo vinavyotengenezwa nchini.
Waziri Mpango pamoja na kupunguza kodi za kampuni kutoka asilimia 30 hadi 10 kwa miaka mitatu ya uzalishaji, pia amefuta rasmi ada ya mwaka ya leseni ya magari huku akisema kwamba uamuzi huo umechukuliwa ili ada hii ilipwe mara moja pale gari linaposajiliwa na baada ya hapo iendelee kulipwa katika ushuru wa bidhaa kama mafuta ya petroli na dizeli.
Katika bajeti iliyowasilishwa, Waziri huyo amependekeza kuondolewa kwa ushuru wa huduma unaotozwa na halmashauri kwenye mabango na vibao vya matangazo vinavyoelekeza mahali zilipo huduma muhimu za kijamii kama vile shule na hospitali huku akitangaza rasmi kuwa kuanzia mwezi Julai mwaka huu, na kwamba Mamlaka ya Mapato (TRA) ndiyo watakaokuwa wakihusika na ukusanyaji wa ushuru wa mabango katika halmashauri zote nchini.
Vilevile bajeti hiyo ya Waziri Mpango imegusa kupunguza ushuru wa mazao kutoka 5% hadi 3% kwa mazao ya biashara na 2% kwa mazao ya chakula na kufuta kabisa ushuru kwa mazao yasiyozidi tani moja yanayosafirishwa kutoka halmashauri moja kwenda nyingine, ikiwa ni pamoja na kupendekeza kutoza ushuru wa forodha kwa 0% badala ya 25% kwenye malighafi kwa ajili ya vifaa vya watu wenye ulemavu, na kufuta ushuru wa huduma kwenye nyumba za kulala wageni ‘Guest House’
Dkt. Mpango ametangaza rasmi ukusanyaji wa kodi ya majengo katika miji na vijiji vyote nchini ambapo amesema majengo/nyumba ambazo hazijafanyiwa uthamini kodi yake itakuwa Shilingi 10,000 kwa nyumba ya kawaida na 50,000 kwa nyumba za ghorofa.
Hata hivyo, Mh. Waziri amesema deni la taifa limeongezeka kwa asilimia 9, kutoka bilioni 39.274 Machi 2016 hadi bilioni 42,883 Machi 2017 huku akiwaodoa hofu watanzania kwamba Tanzania bado ina nafasi ya kuendelea kukopa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.