Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Serikali haitagawa chakula kwa wananchi wavivu ambao hawataki kufanya kazi na kusubiri chakula kutoka serikalini.
Samia ametoa kauli hiyo wakati akihutubia mamia ya wananchi wa Manispaa ya Musoma katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Mukendo mjini hapa.
Mkamu wa Rais amesisitiza kuwa Serikali itapeleka chakula kwa wananchi ambao mazao yao yaliharibiwa kwa mvua au yalikauka kwa ukame au kwa maafa mengine na sio kwa wananchi wanaokaa vijiweni mchana kutwa bila kufanya kazi wakisubiri neema ya chakula kutoka kwa Serikali.
Amewahimiza wananchi kote nchini kuendelea kufanya kwa bidii ikiwemo shughuli za kilimo na pindi wanapovuka wajiwekee akiba na waache tabia ya kuuza mazao yote wanayovuka ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa chakula kwenye familia zao.
Pia aliwataka viongozi wa mkoa wa Mara washirikiane na wananchi katika kuwaelemisha mbinu bora za kilimo ili waweze kupata mazao mengi ikilinganishwa na hali ilivyo kwa sasa.
Makamu wa Rais ametoa mfano kwa mkoa wa Mara kuwa ulikuwa na viwanda vinne vya kuchakata samaki, lakini kutokana na shughuli za uvuvi haramu na wa kutumia sumu umepelekea viwanda vitatu kukosa malighafi hiyo na kusitisha uzalishaji.
Samia alisema jambo hilo ni baya kwa sababu limeikosesha Serikali mapato na kusababisha wananchi wakose ajira kutoka kwenye viwanda hivyo jitihada za makusudi lazima zifanyike katika kukomesha uvuvi haramu katika maeneo mbalimbali nchini hasa katika Ziwa Victoria.