Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbroad Slaa amesema kuwa amesikitishwa sana na kifo cha Mzee Philemon Ndesamburo na kueleza jinsi walivyokijenga chama pamoja.
Dk. Slaa amesema kuwa licha ya Ndesamburo kuwa na utajiri mkubwa, lakini hakuuona kuwa ni kitu bali ni nyenzo ya kuwakomboa wananchi katika sekta mbalimbali.
Dk. Slaa ameitoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja tangu aliyekuwa Mbunge wa Moshi Mjini kwa miaka 15, Mzee Philemon Ndesamburo alipozikwa nyumbani kwake KDC Moshi baada ya kufariki wiki iliyopita alivyopata matatizo ghafla akiwa ofisini kwake.
Dk. Slaa ambaye sasa anaishi Toroto nchini Canada baada ya kujiuzulu wadhifa wake na kuachana na siasa tangu mwaka juzi, alisema kuwa ameshtushwa sana na kifo cha ghafla cha kiongozi huyo tegemeo. Alieleza kuwa licha ya wao kubaki na majonzi, lakini anaamini kazi ya Mungu haina makosa wala haihojiwa.
Aidha, Dk. Slaa alisema kuwa Mzee Ndesamburo alikuwa msikivu na mwenye kuelewa na kuwa tayari kuwasaidia wengi kwa hali na mali kwani mara kadhaa alitoa mali zake kuwasaidia wagombea wa CHADEMA na hata yeye mwenyewe kwenda kuwapigia kampeni bila kujali umbali aliotakiwa kwenda.
Dk. Slaa amesema kuwa kifo hicho ni cha kusikitisha kwa sababu alifariki ghafla, hakupata nafasi ya kuagana na ndugu jamaa na marafiki.