Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad amezindua ofisi mpya za chama hicho katika eneo la Mtaa wa Idrisa Kata ya Mzimuni wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Ofisi hizo kwa ajili ya ya wabunge 40 wa chama hicho ambao wamekosa sehemu ya kufanyia mikutano kutokana na kuzuiwa kuingia ofisi za chama hicho zilizopo Buguruni jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo maalim Seif amesema uamuzi wa wabunge hao kumpatia ofisi ya kufanyia kazi hapo ni cha kiungwana na kinahitajika kuungwa mkono na wanachama wote.
Amesema kwa muda wa miezi 10 sasa wamekuwa wakishindwa kufanya kazi hasa upande wa Tanzania Bara jambo ambalo limewaathiri sana hivyo kupatiwa ofisi kutamsaidia kutimiza majukumu yake vilivyo bila hofu yoyote.
Maalim Seif amesema kukosa ofisi kumewaathiri sana katika baadhi ya mambo hivyo anaamini kwa sasa akifikia Dar es Salaam anamahali pa kukutana na wakurugenzi wake.
Katibu huyo alisema atahakikisha kuwa anaanza kazi haraka iwezekanavyo kwa kukutana na wakurugenzi wake ili waweze kutekeleza majukumu ya chama.
Maalim Seif amesema jitihada zinazofanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukimaliza chama ni kubwa lakini hawataweza kufikia lengo hilo kutokana na misingi ya chama hicho.