Baada ya kuapishwa na kuwa mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro anakabiliwa na changamoto mbali mbali katika kazi yake ya ukuu wa Jeshi  hilo nchini.

Changamoto ya kwanza kabisa iliyo mbele ya Kamanda Sirro ni mauaji ya viongozi wa vijiji na askari Polisi katika wilaya za Rufiji, Kibiti na Mkuranga mkoani Pwani.

Mauaji hayo yanatajwa kuwa ndiyo sababu ya kuondolewa nafasi hiyo aliyekuwa mkuu wa Jeshi nchini, Ernest Mangu ambaye amedumu kwenye nafasi hiyo kwa miaka mitatu baada ya kuteuliwa na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Mrisho Kikwete.

Changamoto nyingine iliyo mbele ya IGP, Sirro ni kurudi kwa kasi ya ujambazi, malalamiko ya vyama vya upinzani kuhusu matumizi ya chombo hiko kwa wanasiasa na kero za wananchi dhidi ya vitendo vya ubakaji na kubambikiwa kesi.

Kamanda Sirro ameteuliwa juzi kushika wadhifa huo akichukua nafasi ya Ernest Mangu ambaye uteuzi wake umetenguliwa na Rais Magufuli.

Kabla ya uteuzi huo IGP Sirro alikuwa kamanda wa Polisi kanda maalum ya Dar es Salaam akichukua nafasi ya Suleiman Kova aliyemaliza muda wake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *