Waziri wa Afya, Mandeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalim amesema kuwa hakuna mgonjwa yoyote aliyehisiwa au kuthibitishwa kuwa na virusi vya ugonjwa wa Ebola hapa nchini.
Kauli hiyo ameitoa leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu taarifa za ugonjwa wa Ebola kuikumba nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambayo tunapakana nayo.
Waziri amesema kuwa hadi sasa hakuna dalili zozote ndani ya Tanzania licha ya ugonjwa huo kuenea nchi jirani ya Congo.
Waziri Ummy amesema kuwa Serikali ya Tanzania inazidi kuchukua tahadhari kuukabili ugonjwa huo kutokana na muingiliano wa wafanyabiashara wa nchi hizi mbili kati ya Tanzania na Congo.
Pia Waziri huyo amewataka wananchi wasiwe na hofu kuhusu ugonjwa huo ila wachukue tahadhari ya ugonjwa huo kutokana upo nchi jirani.
Waziri Ummy amesema kuwa wizara yake inaendelea kushirikiana na sekta mbalimbali katika ufuatiliaji na kutekeleza mikakati ya kudhibiti ugonjwa huo usiingine hapa nchini.