Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amesema marais wastaafu, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete, wanahusika na sakata la mchanga wa madini (makinikia) unaosafirishwa nje ya nchi.
Pia amesema Mkapa na Kikwete hawawezi kukwepa lawama juu ya mchanga huo kwa kuwa mikataba kati ya Serikali na wawekezaji wa migodi inayotajwa, ilisainiwa kwa nyakati tofauti wakati wao wakiwa madarakani.
Kauli hiyo aliitoa mjini Dodoma jana alipozungumza katika mkutano wa Baraza Kuu la Chadema uliokutanisha wajumbe 332, kati ya 370 waliotakiwa kuhudhuria.
Kutokana na hali hiyo, Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema kuna uwezekano mkubwa Kampuni ya Acacia inayomiliki migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu ambako mchanga huo ulipatikana, ikafungua mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro.
Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alisema kwa kuwa uwezo wa Tanzania ni mdogo katika uwekezaji wa miradi mikubwa, Serikali inatakiwa kuwa makini kwa sababu si kweli kwamba wawekezaji wote ni wezi na pia si kweli kwamba wote ni waaminifu.
Akizungumzia hali ya kisiasa, Mbowe alisema katika uzoefu wao kisiasa, Serikali ya awamu ya tano ndiyo ngumu katika harakati zao kwa sababu Rais Magufuli anakandamiza demokrasia.
Kwa mujibu wa Mbowe, alisema serikalini kuna baadhi ya viongozi wanaamini njia pekee ya kuwaweka madarakani ni kuvunja sheria na kuminya demokrasia, jambo ambalo wamelivumilia kwa muda mrefu na kuwafanya viongozi hao waamini Chadema ni waoga.
Alitoa mfano wa matukio aliyosema ni uminywaji wa demokrasia nchini ikiwa ni pamoja na kuzuiwa kwa mikutano ya kisiasa, kukamatwa kwa wanasiasa wa upinzani na kufikishwa mahakamani bila sababu na kupotea kwa kada wa Chadema, Ben Saanane.