Mwanamuziki nyota wa Marekani, Ariana Grande amesema kuwa atasaidia mazishi ya watu 22 waliopoteza maisha kutokana na mlipuko wa bomu mara baada ya kumalizika kwa onyesho lake la muziki nchini Uingereza.
Watu 22 walipoteza maisha na wengine 119 kujeruhiwa kwa tukio la kigaidi la mlipuko wa bomu lililotokea kwenye Ukumbi wa Manchester Arena nchini Uingereza.
Tukio hilo lilitokea wakati akifanya onyesho hilo ikiwa ni ziara yake ya muziki aliyoiita ‘The Dangerous Woman Tour’.
Kupitia akaunti yake ya Instagram, msanii huyo amedai kuungana na familia za watu hao waliopoteza maisha ili atoe mchango wake wa kifedha katika mazishi yao.
Kupitia akaunti yake ya Instagram mwanamuziki huyo ameandika kua “Nimefanya mazungumzo na familia za marehemu na nimewaomba nichangie katika shughuli za mazishi kwa kuwa marehemu wamepatwa na umauti baada ya kuhudhuria onyesho langu, nitaungana nao katika kipindi hiki kigumu kwao,”.