Mzee Francis Maige Ngosha aliyechora nembo ya Taifa amelazwa hospitali ya Muhimbili na matibabu yake yatagharamiwa na Serikali.
Akitoa tamko la serikali Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Khamisi Kigwangalla amesema mzee huyo ambaye ni mmoja wa wachora Nembo ya Taifa wameamua kumuhamishia katika hospital hiyo ya Taifa Muhimbili ili kufanyiwa uchunguzi wa kina na wataalamu wa magonjwa mbalimbali ili kubaini na kutibiwa.
Dkt. Kigwangalla amesema serikali itahakikisha inampa tiba kamili na malezi kwa kuzingatia haki ya kuishi ya binadamu na kuthamini mchango wa wazee na waasisi wa taifa.
Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya dharura kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dkt. Juma Mfinanga amesema wanasubiri majibu ya vipimo wanavyomchunguza na pindi watakapobaini tatizo atapatiwa matibabu yake.
Kwa upande wake Francis Maige Ngosha ambaye ni mmoja wa wachora Nembo ya Taifa ameishukuru serikali na jami iliyokuwa ikimlea kwa miaka yote bila malipo.