Polisi wa Uingereza wamesitisha kubadilishana taarifa za siri na Marekani zinazohusu shambulio la bomu la kujitoa muhanga mjini Manchester lililotokea siku ya Jumatatu.
Hatua hiyo ni kwasababu ya hofu ya kuvuja kwa taarifa hizo katika vyombo vya habari nchini Marekani ambako kunaweza kuzuwia msako wa kumtafuta mtu ambaye huenda amehusika katika utengenezaji wa bomu ambaye hadi sasa hajapatikana.
Iwapo itathibitishwa , hatua hiyo ya kuzuwia kupeana taarifa na mshirika muhimu kabisa wa Uingereza katika ulinzi na usalama kutaonesha kiwango cha hasira ya Uingereza kuhusiana na kuvuja katika vyombo vya habari nchini Marekani kuhusu taarifa za uchunguzi wa polisi.
Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May atalizusha suala hilo wakati wa mkutano wake na rais wa Marekani Donald Trump leo, vyanzo katika serikali vimelieleza shirika la habari la Reuters, baada ya gazeti la New York Times kuchapisha picha za eneo lililotokea mashambulizi mjini Manchester ambako watu 22 waliuwawa.
Picha hizo ni pamoja na mabaki ya bomu linaloshukiwa kutumiwa katika shambulio hilo, mfuko wa kubeba mgongoni uliokuwa umebebwa na mshambuliaji wa kujitoa muhanga na kuonesha damu katika mabaki ya magari yaliyoharibiwa.
Polisi wa Manchester wanamatumaini ya kurejesha uhusiano wa kupashana habari za kijasusi hivi karibuni lakini kwa sasa imekasirishwa.
Baada ya shambulio baya kabisa kuwahi kuwauwa watu nchini Uingereza tangu mwaka 2005, polisi imo katika msako kumtafuta mshirika ambae inashuku alimsaidia Salman Abedi kutengeneza bomu hilo lililowauwa watu 22 siku ya Jumatatu.