Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, Frederick Sumaye amesema kuwa sababu ya kujitoa katika Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB ni kutokana na familia yake kufuatwafuatwa na Serikali.
Baada ya kujitoa kama mmoja wa viongozi wa benki hiyo kubwa nchini, Sumaye amesema kuwa ataendelea kuwa mwanahisa wa benki hiyo ya biashara.
Sumaye amesema kuwa huenda majukumu yake ya kisiasa yakambana na akashindwa kuhudhuria baadhi ya vikao muhimu vya benki hiyo ambavyo ni muhimu kwa ufanisi na ustawi wa benki.
Sumaye ambaye pia ni mjumbe wa Kamati kuu ya Chadema amesema kuwa familia yake imekuwa ikifuatwafuatwa na serikali na kwamba tayari mtoto wake amepokonywa shamba.
Sumaye alinyang’anywa shamba lake lililokuwa Mabwepande kwa madai hakuliendeleza, huku yeye akisema uamuzi wa yeye kupokonywa shamba ulikuwa ni wa kisiasa.
Pia Sumaye amesema kuwa hakuweza kulima shamba hilo kutokana na serikali kupinga kilimo jijini Dar es Salaam.
Sumaye amesema uamuzi wake aliuchukua ili CRDB iweze kuendeshwa na watu walioko huru mbele ya jamii kuepusha hisa za wafanyabishara wengine kuathiriwa.