Wanafunzi watatu ambao ni majeruhi wa ajali ya wanafunzi iliyotokea wilayani Karatu mkoani Arusha wamesafirishwa jana kuelekea Marekani kwa matibabu zaidi.

Wanafunzi hao wamesafirishwa kwa ndege maalumu kutoka jimbo la North Carolina nchini Marekani kwa ajili ya kusafirisha wanafunzi hao.

Ndege hiyo ya Samaritan’s Purse DC 8 N782SP iliwasili Kilimanjaro Tanzania ikiwa na marubani wanne na wahudumu saba tayari kuwabeba majeruhi hao ambao wataambatana na wazazi wao mpaka Marekani kwa matibabu.

Rubani wa ndege hiyo, amewaambia waandishi wa habari kwenye Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA) kwamba baada ya kuondoka, watasimama Cape Verde kuweka mafuta kisha kuelekea Marekani moja kwa moja na wanatarajia kuingia leo.

Ndege hiyo imetolewa na shirika la SAMARITAN’S PURSE linalosimamiwa na mtoto wa mwinjilisti mkubwa wa Marekani, Franklin Graham.

Ndege hiyo imeondoka jana majira ya mchana ikiwa imewabeba watoto hao watatu na mama zao, nesi mmoja na daktari mmoja wa Kitanzania ambao wataendelea kuwahudumia watoto hao ndani ya ndege hiyo yenye uwezo wa kutoa huduma kama ambulance pia.

Ndege hiyo ikishatua North Carolina, SAMARITAN’S PURSE wameandaa ndege nyingine ambayo pia inaweza kufanya kazi kama AMBULANCE na kuwachukua hadi Jimbo la Iowa ambako Hospitali ya Mercy imekubali kuwatibu wagonjwa hao bure kwa muda wote watakaohitaji matibabu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *