Jumla ya watu saba wamepoteza maisha na wengine 10 majeruhi kutokana na athari za mvua ya masika zinazonyesha wilayani Korogwe mkoani Tanga.

Vifo hivyo vyote vimetokana na maporomoko ya maji, mawe, miti na mchanga kutoka katika Milima ya Usambara Magharibi ambavyo vimeendelea kuvamia kwa kasi baadhi ya nyumba zilizo mabondeni katika kata za Mkumbara, Chekereni, Makuyuni, Kwagunda, Kerenge na Ngombezi.

Kutokana na athari hizo hali ya usalama kwa baadhi ya wananchi imekuwa tete hasa wale wanaokaidi agizo la serikali linalowataka kuhama badala yake wanaendelea kung’ang’ania kuishi ndani ya nyumba zao zilizoko bondeni.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Robert Gabriel amesema hali ya uslama kwa wakazi wa maeneo hayo haijatengemaa hivyo jamii inapaswa kufanya kila linalowezekana ili kuokoa maisha.

Mkuu wa Wilaya huyo alitaja athari nyingine zilizopatikana ni kufungwa mara kwa mara kwa baadhi ya barabara kuu na kusababisha baadhi ya magari na watumiaji wengine kusubiri kwa muda wakati maporomoko ya maji na mawe yanapokatiza kwenye maeneo hayo.

Amesema mpaka sasa tathmini halisi ya hasara iliyosababishwa na maafa hayo bado haijapatikana kwa kuwa kamati ya wilaya inatarajia kukutana kesho.

Hata hivyo, alitaja maeneo mengine ambayo yanaendelea kushughulikiwa ni katika barabara kuu ya Mombo – Lushoto ambako vifusi vya udongo vilianguka kutoka juu milimani na kuziba njia katika baadhi maeneo.

Kuhusu barabara kuu ya Tanga – Pangani, alisema Tanroads inafanya juhudi za haraka za kuchepusha barabara katika maeneo yaliyoharibika ikiwemo karibu na daraja la Neema ili kuwezesha watumiaji kuendelea kupata huduma wakati serikali ikiangalia njia ya muda mrefu ya kutengeneza eneo hilo.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *