Serikali imetishia kuifuta kampuni ya Lino International Agency katika uandaaji wa shindano la Miss Tanzania kama itashindwa kutoa zawadi ya gari kwa mshindi wa mwaka jana Diana Edward.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Anastazia Wambura wakati akihitimisha mjadala wa bajeti ya wizara hiyo bungeni juzi mjini Dodoma.
Wambura amesema kuwa kampuni hiyo chini ya Mkurugenzi wake Hashim Lundenga inatakiwa kutoa zawadi kwa mrembo huyo kufikia Juni mwaka huu.
Naibu waziri huyo amesema kama kampuni hiyo itashindwa kutoa zawadi kwa mrembo huyo, hatua kali zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuindoa kuandaa mashindano hayo ya Urembo nchini.
Pia naibu waziri huyo amesema kuwa mbali na Diana, Kampuni hiyo pia inapaswa kuwapa zawadi warembo wengine waliofanya vizuri katika shindano hilo mwaka huu lakini bado hawajapewa stahiki zao.
Diana Edward alitwaa taji la miss Tanzania Oktoba 26 mwaka jana kwenye shindano lililofanyika jijini Mwanza kwa mara ya kwanza.