Mwalimu mkuu msaidizi wa Shule ya Msingi, Lucky Vicent Academy waliokuwa wanasoma wanafunzi 32 waliofariki dunia kwa ajali ya gari jana, Longindo Vicent amesema kuwa yeye ndiyo aliyesimamia safari iliyosababisha vifo vya wanafunzi hao na wafanyakazi watatu.

Mwalimu huyo amesema kuwa wanafunzi hao na walimu wawili walianza safari yao saa 12:30 asubuhi kuelekea Karatu ambapo watoto hao walipaswa kufanya mitihani ya kujipima na Shule ya Tumaini iliyyopo Karatu.

Amesema kuwa Shule hizo mbili zimekuwa na tabia ya kufanya mitihani ya ujirani mwema na hiyo ni mara ya tatu toka waanze kufanya mitihani hiyo.

Wanafunzi hao waliofariki dunia walikuwa wakisoma shule hiyo ya bweni ambapo kwa mujibu wa wakazi wa Arusha wamesema kuwa shule hiyo ni miongoni mwa shule bora mkoani humo ambapo mwaka jana ilitoa mwanafunzi wa kwanza kwa darasa la saba.

Kwa upande wake kamanda wa kikosi cha usalama Barabarani, Mohamed Mpinga amesema kuwa sehemu hiyo gari ilipopata ajali ina kona nyingi na mteremko mkali sana na kwamba kuna sehemu ajali inatokea kutokana na miundombinu yake ilivyokaa.

Pia mkuu wa wilaya ya Arusha, Gabriel Daqaro amesema kuwa miili ya wanafunzi hao itaagwa leo katika uwanja wa Shekh Amri Abeid jijini Arusha.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *