Vyombo vya habari za Korea Kaskazini vimesema kuwa maajenti wa Marekani na Korea Kusini wanapanga njama ya kumuua kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un.

Taarifa kutoka wizara ya usalama nchini Korea Kusini imesema mawakala wa kundi la kigaidi linaloungwa mkono na Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) na shirika la ujasusi la Korea Kusini wameingia nchini Korea Kaskazini kwa nia ya kumuua kiongozi huyo.

Taarifa hiyo imesema Korea Kaskazini itawasaka mawakala hao na kuwaangamiza bila huruma huku wasiwasi ikiendelea kuongezeka katika rasi ya Korea.

Taarifa hiyo, ambayo imechapishwa na shirika la habari la Korea Kaskazini inasema njama hiyo inahusisha kutumiwa kwa silaha ya bio-kemikali pamoja na kemikali yenye miali nururishi na sumu.

Matokeo ya shambulio kama hilo yataanza kubainika baada ya miezi sita hadi 12, taarifa hiyo imesema.

Vita vya maneno kati ya Marekani na Korea Kaskazini vimezidi wiki za karibuni huku Korea Kaskazini imetishia kufanya jaribio la sita la silaha za nyuklia.

Hali ya wasiwasi imekuwa ikiongezeka siku za karibuni, huku Korea Kaskazini na Kusini zikifanya mazoezi ya kijeshi.

Mwishoni mwa wiki, Rais Marekani Donald Trump alisema angependa kukutana na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un, iwapo kungekuwa na mazingira mahsusi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *