Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin William Mkapa amepongeza utendaji wa kazi wa Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Katika pongezi hizo Mkapa amepongeza zoezi la kuwaondoa wafanyakazi hewa na wenye vyeti feki baada ya kufanyika zoezi la uhakiki na kubaini wafanyakazi hewa kwenye sekta mbali mbali za umma nchini.
Rais huyo mstaafu amesema kuwa jambo hilo ni jema kutokana watumishi hao walikuwa wanaingizia hasara serikali kutokana na kupokea mishahara ya Serikali.
Mkapa amesema hayo wakati wa mahojiano na Shirika la utangazaji la Ujerumani (DW) huku akisema kuwa anajilaumu kwanini yeye hakufanya hivyo wakati wa utawala wake.
Kauli hiyo ya Mkapa imekuja baada ya watumishi 9,932 kubainiki kufoji vyeti vya elimu na kuamuriwa kuondoka kwenye nafasi zao za kazi.