Waziri Masuala ya Jamii na Kazi nchini Somalia, Abas Abdullahi Siraji ameuawa kwa kupigwa risasi mjini Mogadishu muda mchache baada ya kuzindua mradi wa ujenzi wa jengo kwa ajili ya watumishi wa umma.
Waziri huyo kijana aliyekuwa na miaka 31 ameuawa karibia na ikulu ya Rais nchini Somalia baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana akiwa ndani ya gari lake.
Abas Abdullahi Sheikh Siraji hakuwa waziri wa kawaida nchini Somalia kwani alipata umaarufu mkubwa baada ya kushinda kiti cha ubunge na kuiwakilisha Jubbaland.
Amewahi kuishi katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab iliyopo nchi ya Kenya akiwa mtoto na kisha kurejea nchini mwake mwaka jana alipokwenda kwa ajili ya uchaguzi mkuu.
Alikuwa waziri wa masuala ya jamii na kazi huku watu wengi wakimtaja kama mtu machachari sana miongoni mwa mawaziri.
Waziri wa habari wa Somalia amesema kuwa washukiwa wa mauaji hayo wamekamatwa na sheria itachukua mkondo wake.