Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amemtahadharisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, John Wanga endapo atashindwa kusimamia vema agizo la urasimishaji makazi holela na uandaaji wa hati miliki kwa wananchi atatumbuliwa.

Alitoa tahadhari hiyo juzi baada ya kusomewa taarifa ya utekelezaji wa   urasimishaji na uandaaji wa hati za ardhi ambako Halmashauri ya Ilemela imetekeleza kwa asilimia moja kwa kuandaa hati 834 huku viwanja  vingine 16,000  vikiwa vimepimwa bila kuandaliwa hati.

 Lukuvi  ambaye alionekana kukasirishwa na hali hiyo alisema kushindwa kuandaliwa    hati hizo  ndani ya Halmashauri ya Ilemela ambayo ina maofisa ardhi  na watathmini zaidi ya 40 kmeisababishia  hasara   Serikali.

Alisema kazi hiyo ingefanyika ilivyotarajiwa serikali ingepata  mapato ya  Sh bilioni 2.5 kwa mwaka lakini kilichopatikana  ni Sh bilioni 1.3 tu.

Waziri alisema Halmashauri za Ilemela na Nyamagana  zinatakiwa zikamilishe hatua hiyo  Juni 30, mwaka huu atakapoifunga rasmi na kutangaza ‘masterplan’ ya Jiji la Mwanza ifikapo Agosti.

Aliwataka wananchi kutambua kuwa baada ya kufungwa  urasimishaji makazi haitatokea   tena  fursa ya namna hiyo.

Amesema wananchi ambao hawatakuwa na hati ya eneo analoishi watahesabika kama wavamizi, hivyo watapoteza haki yao na maeneo hayo yatachukuliwa na Serikali kwa shughuli nyingine.

Lukuvi amesema Serikali kuu imetenga Sh bilioni 22 kwa ajili ya masterplan ya   Mwanza ambayo itaanza kutekelezwa Agosti mwaka huu,  kazi ambayo  itafanywa na wataalamu kutoka China.

Source: Mtanzania

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *