Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa ametangaza rasmi kumuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta.

Kenyatta aliyeunga ushirika pamoja na William Rutto,  anaingia katika kinyang’anyiro cha kuwania awamu ya pili ya kuiongoza Kenya huku upande wa upinzani ukiwa umepitisha jina la Raila Odinga kupeperusha bendera ya upinzani.

Wakati Lowassa akitangaza kumuunga mkono Kenyatta, kwa upande wake Odinga tayari ilishajulikana wazi urafiki wake na Rais Dk. John Magufuli ambao umeanza miaka mingi tangu akiwa Waziri wa Ujenzi.

Hatua hiyo ya Lowassa ambaye anatajwa kuwa mwanasiasa mwenye ushawishi nchini na Afrika Mashariki imekuja baada ya kutembelewa jana nyumbani kwake Monduli na wabunge zaidi ya 20 na maofisa kutoka Kaunti ya Kajiado nchini Kenya.

 Alisema ushawishi wake kwa Kenyatta umejengwa na imani kubwa aliyonayo kwa Rais huyo akiamini kwa dhati kwamba ana uwezo mkubwa wa kuwaunganisha wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na hasa Tanzania na Kenya.

Katika tamko lake, Lowassa mwanasiasa mwenye ushawishi nchini Kenya pia kupitia jamii ya Kimaasai aliwasihi wananchi wa Kenya kutokufanya makosa katika uchaguzi ujao.

Source: Mtanzania

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *