Klabu ya Simba imeapa kufa na Azam baada ya kuona njia pekee itakayowasaidia kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao ni kunyakua taji la Kombe la FA.

Simba ambayo imeingia hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho kwa kuitoa Madini FC ya mkoani Arusha, watavaana na Azam Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wekundu hao wa Msimbazi wanajua kile wanachopaswa kufanya dhidi ya Azam kwani kupoteza mchezo huo itakuwa wameondolewa moja kwa moja kwenye ndoto zao za kushiriki michuano ya kimataifa hapo mwakani kwa kuwa kwenye ligi tayari Yanga wana nafasi kubwa ya kutetea taji lao.

Kwa upande wake kocha msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja amesema wanajiandaa vya kutosha kuhakikisha wanasonga mbele kwenye mchezo huo.

Akizungumzia kurejea kwa beki Abdi Banda aliyetoka kifungoni baada kufutiwa adhabu kwa kosa la kumpiga ngumi kiungo wa Kagera Sugar, George Kavila na Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji, Mayanja alisema hilo limewaongezea nguvu kikosini na kwa sasa wanachofanya ni kurekebisha makosa kwenye kikosi chao.

Simba inaongoza ligi ikiwa na pointi 59 imepoteza matumaini ya ubingwa baada ya kubakiwa na michezo mitatu huku wapinzani wao Yanga wanaoshika nafasi ya pili wakiwa na michezo mitano ambapo kama wakishinda zote watakuwa tayari wamejihakikishia ubingwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *