Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Vyombo Vya Habari yatakayofanyika Mei 2 na 3 mwaka huu.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Salome Kitomari amesema kuwa maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika katika Ukumbi wa Malaika Beach Resort iliyoko jijini Mwanza.
Akielezea juu ya maadhimisho hayo amesema kuwa wanatarajiwa kuwepo wadau mbalimbali na watazungumzia masuala yanayohusu Uhuru wa vyombo vya Habari na wanahabari kwa ujumla.
Pia amesema kuwa lengo lingine ni kufikia makubaliano ya kitaifa juu ya kuanzisha utaratibu wa usalama na ulinzi wa wanahabari na waandishi wa habari wa mitandao na nje ya mitandao.
Ameongeza kwa kusema kuwa lengo lingine ni kutetea sera na mageuzi ya kisheria kwaajili ya vyombo vya habari na maendeleo endelevu.