Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole amesema kuwa Nape Nnauye anapaswa kucuhukuliwa hatua na kamati ya maadili ya CCM kutokana na kauli yake kuwa alisaidia kukitoa chama hicho shimoni.
Polepole amesema kuwa kauli hiyo ya Nape sio kauli sahihi ya kiongozi na kwamba yeye pekee hawezi kukitoa chama shimoni huku kukiwa na wanachama milioni nane na maelfu ya viongozi.
Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi wa CCM alisema kuwa Kamati ya Maadili inapaswa kuliangalia suala hili na kumchukulia hatua Nape.
Polepole amesema kuwa hatua zinazopaswa kuchukuliwa kwa viongozi kama Nape sio za kuwawekea ukomo bali kuwalea kimaadili kwa kutumia hekima na busara ili watambue kuwa chama sio punda anayeweza kutumbukia shimoni.
Pia ameongeza kwa kusema kuwa CCM iko kwenye mpango wa kuanzisha chuo kikuu kitakachotoa mafunzo kwa makada wake kuhusu nidhamu na maadili.
Nape alitoa kauli hiyo dakika chache baada ya mkutano wake na waandishi wa habari kuzuiwa na kutishiwa bastola na mtu mmoja baada ya kuondolewa kwenye nafasi ya Uwaziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.