Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro amesema kuwa wamewakamata watuhumiwa watano wanaotuhumiwa kufanya fujo katika mkutano wa chama cha wananchi (CUF).
Watu hao baada ya kuvamia mkutano huo wamesababisha baadhi ya watu kujeruhiwa kutokana na wavamizi hao kuwa silaha za bastola na mapanga.
Kamishna Sirro amesema hayo leo wakati akizungumza na wandishi habari katika Hoteli ya Vinna iliyopo Mabibo jijini Dar es Salaam.
Kamanda Sirro amesema jeshi lake lilipokea taarifa ya kuvamiwa kwa Mkutano wa wanachama wa CUF ambapo baada ya taarifa hizo jeshi lake lilifanikiwa kuwakamata jumla ya watuhumiwa watano wanaodaiwa kushiriki katika tukio hilo.
Pia Sirro ameaeleza kuwa watuhumiwa hao wanaendelea kuhojiwa na pindi upelelezi utakapokamilika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Vilevile ameeleza juu ya baadhi ya watu wanatumia vibaya jina lake hasa nyakati za usiku kwa madai ya kuwa amewaatuma yeye kwa masuala ya migogoro ya kisiasa.
Aidha amefafanua kuwa masuala ya kisiasa siyo jukumu lake kimsingi yeye ni mtumishi wa serikali anayehusika na masuala ya ulinzi na uslama wa raia si vinginevyo, hivyo akawataka wanaofanya hivyo waache tabia hiyo mara moja.