Jeshi la polisi mkoani Pwani limewaua kwa kuwapiga risasi watu watatu wanaodhaniwa kuhusika na mauaji ya viongozi wa vijiji na vitongoji na askari polisi katika wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji mkoani Pwani.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani Onesmo Lyanga katika taarifa yake amedai kuwa watu hao wamefariki dunia wakati wakipelekwa hospitali ya Mission ya Mchukwi kwa matibabu baada ya kujeruhiwa kwa risasi miguuni na kiunoni walipojaribu kukimbilia porini wakiwa kwenye pikipiki baada ya kukaidi amri halali ya polisi iliyowataka wasimame kutokana na kuwatilia mashaka.
Lyanga amesema polisi waliokuwa katika doria walipata taarifa kutoka kwa wasafiri kuwa waliona pikipiki tatu zilizokuwa zinatokea Kibiti kupitia barabara kuu ya Dar es salaam -Lindi zimepakia watu watatu kila moja na pikipiki mbili kati ya hizo ziliwabeba waliovalia hijabu ndipo walipowapa taarifa askari wa usalam barabararni walioko katika kizuizi cha Mparange ili wawasimamishe na kuwatambua lakini hawakutii amri.
Kamanda Lyanga alizidi kueleza kuwa askari wa kituo cha Mwembe, Muhoro waliwasimamisha lakini hawakutii amri na kuongeza kasi, ndipo askari waliwafuatilia hadi kuvuka daraja la Mkapa na wakatoa onyo kwa kufyatua risasi hewani lakini waliendelea kukaidi amri.
Baadaye watu hao waliamua kuruka kutoka kwenye pikipiki zao na kukimbilia msituni, kitendo kilichowafanya polisi kuwafyatulia risasi za miguuni na kiunoni na kuwakamata lakini walifariki dunia wakati wakikimbizwa hospitali ya Mission ya Mchukwi ambako daktari alithibitisha watu hao walikuwa wameshafariki
Kamanda amesema majeruhi hao waliovalia hijabu baadaye walitambulika walikuwa wanaune waliotumia pikipiki aina ya boxer yenye namba za usajili MC 272 BLW.