Shirikisho la soka nchini (TFF) limemfungulia mashtaka ya kinidhamu Msemaji wa klabu ya Simba, Haji Manara kwenye Kamati ya Maadili baada ya kulishtumu shirikisho hilo.
Taarifa iliyotolewa na shirikisho hilo imesema kuwa Manara atapewa mashtaka yake leo na kujulishwa lini na wapi yatasikilizwa mashtaka hayo.
Taarifa hiyo ya TFF imesema kuwa “Kwa mujibu wa Katiba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kila mwanafamilia wa mpira wa miguu Tanzania analazimika kuheshimu na kufuata kanuni za maadili za shirikisho kama zilivyoainishwa kwenye kanuni zake mbali mbali.
Taarifa hiyo imesema kuwa TFF inaendelea kutoa rai kwa wadau wa mpira kuwa pamoja ni kwamba ni haki yao kushauri, kupendekeza, kukosoa lakini yote haya yafanyike kwa staha ili kutunza heshima ya mpira wetu.
Siku ya Jumatano Manara alizungumza na waandishi wa habari kuhusu sakata la pointi 3 za Simba na Kagera Sugar, ambapo aliishushia tuhuma nzito TFF hasa viongozi wake wakuu Jamal Malinzi na Celestine Mwesigwa kuwa lengo lao ni kuibeba Yanga na kuikandamiza Simba.