Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).

Katika mazungumzo hayo Rais Magufuli amewahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendeleza na kuimarisha zaidi ushirikiano kati yake na wafanyakazi

Rais Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika kikao na Viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (Trade Union Congress of Tanzania -TUCTA) Ikulu jijini Dar es Salaam.

Katika Mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, Mheshimiwa Rais Magufuli amesema pamoja na kuimarisha ushirikiano huo, Serikali ipo tayari kupokea maoni na ushauri wowote utakaotolewa na vyama vya wafanyakazi wenye lengo la kuboresha maslahi ya wafanyakazi na kuongeza tija kazini.

Rais Magufuli amesema Serikali inatambua changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi na itaendelea kuchukua hatua za kukabiliana nazo kama ambavyo imeanza kufanya hivyo.

Kwa upande wao Viongozi wa TUCTA wakiongozwa na Rais wa Shirikisho hilo Bw. Tumaini Nyamhokya wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi kubwa zinazochukuliwa na Serikali yake kujenga uchumi imara, kuimarisha utendaji kazi wa watumishi wa Serikali, kupambana na rushwa, kuondoa watumishi hewa na kulipa madeni ya watumishi.

Viongozi hao wameahidi kushirikiana na Serikali katika kusimamia haki na wajibu wa wafanyakazi na wameomba Serikali iendelee kufanyia kazi masuala mbalimbali ya wafanyakazi ikiwemo kuwalipa stahili zao na kuboresha mazingira ya kazi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *