Sakata la watumishi wa umma kushughi vyeti vya elimu limezidi kuchukua sura mpya na sasa wamefikia zaidi ya 10,000.

Hatua hiyo, inatokana na uhakiki uliofanywa na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ambayo imebaini waombaji kazi 39,511 kati yao, 1,951 wana vyeti vya kughushi.

Kuongezeka kwa idadi hiyo, kunatokana na kauli ya Rais Dk. John Magufuli, wiki iliyopita, kwamba anasubiri ripoti ya wafanyakazi wa Serikali ambao wamebainika kuwa na vyeti feki.

Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam, wakati akizindua mabweni mapya ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Alisema anafahamu idadi ya watumishi wenye vyeti feki ni zaidi ya 9,000 na anaisubiri ripoti hiyo kuifanyia kazi.

Akiwasilisha hotuba ya bajeti ya mwaka 2017/18 kwa ofisi yake jana bungeni mjini hapa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki, alisema baada ya kubainika kwa hali hiyo, wahusika waliondolewa kwenye mchakato, huku vyeti hivyo vikiwasilishwa katika mamlaka husika kwa hatua za kisheria.

Hata hivyo, zipo taarifa zinazodai kuwa orodha ya watumishi wa umma ambao wamebainika kuwa na vyeti feki itawekwa hadharani Aprili 30.

Zaidi inaelezwa kuwa sakata hilo la vyeti feki linawagusa pia mabalozi ambao ni wawakilishi wa Watanzania katika mataifa mbalimbali, wakuu wa wilaya na mikoa.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *