Kesi ya kujeruhi na unyang’anyi wa kutumia silaha inayomkabili Salum Njwete ‘Scorpion’, anayedaiwa kumjeruhi kwa kumchoma visu na kumsababishia upofu Said Mrisho, jana imeshindwa kuendelea baada ya shahidi upande wa Jamhuri kushindwa kutokea mahakamani.
Katika viunga vya Mahakama ya Wilaya ya Ilala, kama kawaida umati uliokuwa ukitaka kusikiliza kesi hiyo ulifurika mapema asubuhi kutaka kujua kinachoendelea.
Scorpion alifikishwa mahakamani hapo akitokea Gereza la Ukonga na kuhifadhiwa kwa muda kwenye mahabusu ya mahakama hiyo.
Majira ya saa nne kamili chumba cha mahakama kilikuwa tayari kimeandaliwa kwa ajili ya kesi hiyo ambapo Wakili wa Scorpion, Juma Nasoro, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Nasoro Katuga, Hakimu anayeendesha kesi hiyo, Frola Haule na makarani wote walikuwa tayari kwenye chumba inapoendeshwa kesi hiyo wakimsubiri mtuhumiwa huyo apelekwe ili kesi iendelee.
Baadaye maafande wa magereza zaidi ya nane wengine wakiwa na silaha walimchomoa Scorpion na kumpeleka kwenye chumba cha mashitaka mbele ya hakimu, Frola Haule.
Scorpion akiwa kizimbani, Wakili Katuga aliiambia mahakama hiyo kuwa kesi hiyo ilifika mahakamani hapo kwa ajili ya shahidi wa nane upande wa Jamhuri kutoa ushahidi wake.
Wakili huyo alisema shahidi huyo alitoa udhuru mahakani hapo kuwa asingeweza kufika mahakamani hapo kwa kuwa anaumwa.
Baada ya ombi la wakili huyo, mahakama hiyo iliahirisha kesi hiyo mpaka Mei 2 mwaka huu ambapo Scorpion alirudishwa rumande.