Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi kuu Tanzania Bara imefanya kikao chake siku ya Ijumaa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupitia malalamiko ya Simba dhidi ya Kagera Sugar.
Klabu ya Simba iliwasilisha malalamiko ikitaka ipewe ushindi wa pointi tatu na mabao matatu kutokana na timu ya Kagera Sugar kumchezesha mchezaji Mohamed Fakhi Gharib wakati akiwa na kadi tatu za njano katika mechi yao namba 194 iliyofanyika Aprili 2, 2017 Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Kamati baada ya kupitia malalamiko hayo, imeahirisha shauri hilo hadi Alhamisi Aprili 13, 2017 kwa vile bado inafuatilia baadhi ya vielelezo kuhusu malalamiko hayo kabla ya kufanya uamuzi.
Kamati hiyo endapo ikijiridhisha Simba inaweza kupewa points Tatu na magoli matatu baada ya kosa hilo la Kagera Sugar kufanya kosa hilo la kumchezesha mchezaji huyo, Mohamed Fakhi.
Katika mechi hiyo Simba ilifungwa goli 2-1 na Kagera Sugar kwenye mechi iliyofanyika katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.